13 Aprili 2015

Butiku: Si dhambi kupigia Katiba kura ya hapana

Mbeya. Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku amesema si dhambi kwa wananchi kupiga kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa.
Akizungumza juzi jioni kwenye mdahalo wa Katiba ulioandaliwa na taasisi hiyo ambao ulifanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (Teku) jijini Mbeya, Butiku alisema kura ya Hapana au Ndiyo, zote zinatoa fursa sawa kwa wananchi kuamua kwa utashi wao.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na mamia ya wakazi wa Mbeya, Butiku aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, alieleza kuwashangaa viongozi wa vyama na Serikali kuwachagulia wananchi kura ya Ndiyo.
Akitolea mfano wa chama chake cha CCM, Butiku alisema hakitakiwi kuwahadaa Watanzania na kuwataka kuipigia kura ya Ndiyo katiba hiyo, badala yake kiwaache waamue wenyewe.
Aliwataka wananchi watumie muda huu kuitafuta nakala ya Katiba Inayopendekezwa, waisome na kuielewa ili hatimaye waamue ama kuipigia kura ya Hapana au Ndiyo.
“Mchakato huu una mambo makuu mawili ya kuamua ambayo ni kura ya Ndiyo au Hapana. Hivyo basi kupiga kura ya Hapana siyo dhambi kwani inatoa nafasi kwetu sote kukaa tena na kuangalia upungufu uliojitokeza na kilichosababisha upungufu huo nini ili tusirudie tena makosa,” alisema Butiku na kuongeza:
“Kura ya ndiyo inamaanisha tunaikubali Katiba Inayopendekezwa, hata ikiwa haina mashiko itaendelea kutumika kwa vile mmeikubali, lakini nisisitize kwamba kura ya hapana siyo dhambi, ipo kisheria na asije mtu akawaambia mpigie kura ya ndiyo.
Alisema kabla ya kuipitisha au kuikataa Katiba Inayopendekezwa ni vyema ikashindaniwa kwa hoja na si kwa nguvu au ngumi huku akiwataka vijana nchini kutothubutu kujiingiza kwenye mikumbo inayoweza kusababisha nchi ikaingia kwenye machafuko.
Profesa Baregu
Akizungumza katika mkutano huo, Profesa Mwesiga Baregu ambaye pia alikuwa mjumbe wa tume hiyo, alisema licha ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuahirisha Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendelezwa kwa muda usiojulikana, kwa mtazamo wake anaona haitakuwapo kabisa.
“Mimi Baregu, nasema hivi siyo kwamba imeahirishwa, nafikiri haitakuwapo kabisa kura hiyo na hii inatokana na ambavyo mchakato mzima ulivyoendeshwa na si kwa maudhui yaliyomo kwenye Katiba Inayopendekezwa, bali ni kwa namna ambavyo Bunge Maalumu la Katiba lilivyofanya na uandishi wake.”
Alisema katu Watanzania wasije wakawa na papara na Katiba hiyo hata baada ya Uchaguzi Mkuu, bali wawe na subira kwani wakiiendea haraka inaweza ikaipeleka nchi mahala pabaya na kujikuta ikitumbukia kwenye machafuko yasiyo na tija.
Hamphrey Polepole
Mjumbe mwingine wa tume hiyo, Hamphrey Polepole alisema Watanzania wanatakiwa kutambua kwamba Katiba siyo kitu cha kuamuliwa na wanasiasa au kuamua kwa kusikia tu, bali ni kwa kushiriki katika kuipigia kura ya hapana au ndiyo kwa kutumia utashi wao binafsi.
“Katiba hii siyo ya wanasiasa ni ya wananchi wenyewe, lakini cha kushangaza hapa ni wanasiasa wanavyochukua nafasi kubwa ya kuuteka mchakato huu na hii yote wanataka wapate nafasi ya kulinda masilahi yao na kuendelea kututawala watakavyo, hivyo ndugu zangu wa Mbeya na Watanzania wote chukueni hatua.”
Alisema anawashangaa hata viongozi wakubwa ndani ya vyama na Serikali kuendelea kuipigia ‘debe’ Katiba Inayopendekezwa kwa kuwahadaa wananchi kupiga kura ya ndiyo wakati wakitambua fika kwamba haijakidhi matakwa Watanzania.
Mjumbe mwingine wa iliyokuwa Tume hiyo, Ally Saleh alizungumzia masuala ya muundo wa Serikali, alishangiliwa na mamia ya watu waliofurika ukumbini hapo aliposema: “Mwenyekiti wangu hapa (Butiku) kasema kwamba kura ya hapana siyo dhambi, lakini mimi nasema hivi, watu wasipige kabisa kura.”

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

KUWEKA TANGAZO LAKO HAPA NI BEI NAFUU
KUWEKA TANGAZO LAKO HAPA NI BEI NAFUU

TANGAZO LA KAZI -Commited youth agricultural organisation CYAO is looking for a person who is specialised in agriculture

POSITION DESRIPTION;

Agricultural Technician

Qualifications

Diploma in agriculture

Mode of application applicant must send an updated Cv,birth cirtificate,one recent passport size, an accademic cirtificate, age limit 20 to 35

apply to Project cordinator,Commited youth agriculture organisation,P.O.Box 78438 Dar es salaam or you can call through +255657990920/+255754823728