Dar es Salaam. Uhakika wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutamba
katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba utategemea umahiri wake katika
kukabiliana na vikwazo sita vinaonekana kuwa mwiba kwake ambavyo
upinzani kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), unatarajiwa
kuvitumia kama mtaji wake katika kampeni.
Vikwazo hivyo ni kuwapo kwa makundi ndani ya CCM
yanayotokana na mitandao ya urais, hasira za wananchi juu ya mchakato wa
Katiba Mpya, tuhuma za ufisadi ama kwa makada au Serikali yake, suala
la Mahakama ya Kadhi, ahadi za Rais 2010 ambazo hazijatekelezeka na
kuimarika kwa upinzani na muungano wake wa Ukawa.
Hata hivyo, baadhi ya makada wa chama hicho bado
wanaona kuwa pamoja na vikwazo hivyo, chama hicho kitapenya katika
uchaguzi huo na kuongoza tena Dola kwa kuwa kinao mtaji mkubwa wa
wanachama na mtandao wake ni mpana kuliko chama chochote nchini.
Mgawanyiko na makundi
Kwa nyakati tofauti, viongozi wa CCM kupitia vikao
vya ndani na mikutano ya hadhara, wamekuwa wakizungumzia jinsi ya
kudhibiti mivutano ya makundi ya urais miongoni mwa wanachama wake,
tatizo kubwa likiwa ni jinsi gani ya kuwaleta pamoja na kuponya makovu
baada ya uteuzi.
Mathalani, tangu uchaguzi mkuu uliopita, viongozi
wa CCM wamekuwa wakieleza mgawanyiko baada ya uteuzi kama sababu ya
kuyakosa baadhi ya majimbo muhimu nchini na tatizo hilo linaweza
kukikumba hata ngazi ya urais, kisipokuwa makini.
Makundi ya watia nia ya urais kwa sasa yamesambaa
mikoani kimyakimya kutafuta uungwaji mkono na baadhi yake yamejijengea
ushindani wa kihasama kati ya kundi moja na jingine hadi kutupiana
maneno makali na tuhuma mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, jambo
ambalo linaweza kuhatarisha uimara wa chama na kukiathiri katika
uchaguzi wa Oktoba.
Mchakato wa Katiba
Tangu ulipoanza mchakato huo hadi sintofahamu
inayoendelea ya Kura ya Maoni, yametokea mambo mengi na kuzua hasira kwa
baadhi ya Watanzania, hivyo kuwa miongoni mwa mambo yanayohofiwa
kutumika kama bakora ya kuiadhibu CCM katika Uchaguzi Mkuu.
Hasira hiyo inatokana na jinsi wananchi
walivyoipokea na kuiamini Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na
Jaji Joseph Warioba na kuyakubali matokeo ya kazi yake lakini baadaye
yakapinduliwa na Bunge la Katiba, kwa wingi wa kura za wajumbe wa CCM,
ambazo hadi leo bado zinatia shaka.
Hata kitendo cha kushindikana kwa karata ya
Serikali kuitisha Kura ya Maoni Aprili 30, ni kikwazo kingine kwa chama
hicho, kwa kuwa hakuna namna nyingine ya kuonyesha kuungwa mkono na
umma, ikiwa ni siku chache baada ya nguvu yake kuonekana kupungua katika
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Ufisadi
Haitoshi, katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Serikali
imekuwa kwenye kipindi kigumu cha matukio ya ufisadi yaliyosababishwa na
ama watendaji au makada wake. Miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na
sakata la Richmond ambavyo kwa vyovyote mwaka huu, litaibuka kwa kuwa
linahusishwa na baadhi ya wagombea, sakata la uchotwaji wa fedha katika
Akaunti ya Tegeta Escrow ambalo bado ni bichi, Epa ambayo baadhi ya
watuhumiwa walisamehewa baada ya kurejesha fedha ambazo hazikuelezwa
bayana zilikopelekwa na matukio yasiyokoma yanayoibuliwa katika ripoti
za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Nguvu ya upinzani
Matokeo ya upinzani katika Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa 2014 nayo yanaonekana kujenga hofu kwa CCM kwa kuwa yameibua
picha mpya kuwa vyama vya upinzani vinakubalika hadi vijijini ambako
chama hicho kimekuwa kinazoa kura bila upinzani.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, ushindi wa CCM
umepungua kutoka zaidi ya asilimia 91 za uchaguzi wa 2009 hadi asilimia
70 katika mitaa na vijiji mwaka jana, jambo ambalo lisipoangaliwa
linaweza kukiathiri chama hicho.
Ahadi zisizokamilika
Mambo mengine mwiba kwa CCM kama chama tawala ni
baadhi ya ahadi za 2010 ambazo hazijakamilika, zikiwamo za ilani ya
uchaguzi na nyingine alizotoa Rais Jakaya Kikwete binafsi kadri
alivyokuwa anaona mahitaji ya wananchi katika kampeni zake.
Baadhi ya ahadi hizo ni meli katika baadhi ya maziwa, barabara, vivuko, madaraja, hospitali na huduma nyingine mbalimbali.
Mahakama ya Kadhi
Pengine suala ambalo limeacha kovu kubwa katika
uso wa CCM ni suala la Mahakama ya Kadhi. Suala hili liliingizwa katika
ilani yake ya 2005 kuwa ikishinda itatafuta suluhisho ambalo hadi leo
limeshindikana, badala yake likaweka ufa mkubwa katika utengamano wa
Taifa.
Katika siku za karibuni, Waislamu walishuhudiwa
wakidai ahadi hiyo iingizwe kwenye Katiba Mpya, lakini Serikali ikaomba
isiwemo, ikisema itatungiwa sheria ambayo hata hivyo inapingwa na
viongozi wa Kikristo wanaodai Serikali haina dini hivyo isijihusishe
nayo. Muswada huo tayari umewasilishwa na kuondolewa bungeni mara mbili.
Maoni ya wachambuzi
Akizungumza vikwazo hivyo, Profesa Gaudence
Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha, aliungana na gazeti hili, akisema
kashfa serikalini kwa vyovyote utakuwa ni mtaji mkubwa kwa Ukawa katika
Uchaguzi Mkuu ujao.
Alisema suala la Katiba ni kesi inayojitegemea kwa Watanzania
wengi wasiokubaliana na uamuzi wa Serikali kulazimisha muundo wa
Serikali mbili ikiwa ni tofauti na maoni yaliyokusanywa na Tume ya Jaji
Warioba.
“Kuna athari za escrow ambazo zimeanza kuonekana
tangu uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hakuna aliyetegemea matokeo yale
kwa upinzani, kwa hivyo hali siyo nzuri mpaka baadhi ya maeneo ya
vijijini,” alisema na kuongeza:
“Hali ni mbaya katika tathmini inayoonekana kwa
sasa na kama asingekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana chama
hicho kisingekuwa na dalili za kurudi Ikulu katika Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba, Kinana ameiombea CCM msamaha na kwa kiwango fulani ameibeba.”
Hata hivyo, Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na
Utawala, Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Emmanuel Mallya alisema
vikwazo hivyo, haviwezi kuwa kipimo pekee cha kuikwamisha CCM kutokana
na uzoefu uliopo.
“Kuna makundi matatu ninayoyajua, kuna Watanzania
ambao huwezi kuwabadili kitu kwa CCM, wataichagua tu bila kujali
changamoto hizo. Pili, kuna kundi la vijana ambao hufanya uamuzi dakika
za mwisho, hawajulikani, kuna kundi la vijana la mabadiliko na kundi la
kina mama wanaoangalia upepo wa utulivu, hawa hupiga kura kwenye utulivu
wa chama,” alisema Dk Mallya.
Alisema Serikali bado inayo nafasi kubwa ya
kutafuta maridhiano na taasisi, mashirika na makundi mbalimbali kwenye
jamii ili kuondoa athari zinazoweza kujitokeza katika Uchaguzi Mkuu.
Dk Mallya alisema masuala ya Mahakama ya Kadhi na
Mchakato wa Katiba yanaweza kuwa na athari kubwa kwa CCM kwa wananchi
kupigia kura vyama vya upinzani.
“Serikali inaweza kurejesha imani ya Watanzania
hata kwa muda uliobakia endapo itakubali kujadiliana, kukubaliana na
taasisi, mashirika, viongozi wa dini na wadau,” alisema Dk Mallya.
Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Penina Mlama alisema suala la
Katiba limewakatisha tamaa Watanzania wengi waliokuwa wameweka maoni yao
na kuondolewa.
Profesa Penina alisema mchakato wa Katiba ulikuwa
na matarajio mazuri kwa Watanzania lakini jinsi ulivyochakachuliwa,
umewafanya wengi kugawanyika.
“Sasa siwezi kujua kama hatua hiyo inaweza kuwa ni
hasira ya kuiadhibu CCM, hilo sijui, ila kwa kweli imewakatisha tamaa
sana, labda tusubiri tuone,” alisema Profesa Mlama.
Kauli ya CCM
Kupitia ziara zake za ujenzi wa chama, Kinana amekuwa akisema asilimia 90 ya ahadi za 2010 zimeshatekelezwa.
Siku chache zilizopita, Katibu wa Itikadi na
Uenezi, Nape Nnauye alilieleza gazeti hili kwamba, hata kama Ukawa
wangeunganisha vyama vyote vya upinzani, bado CCM itakuwa na mtaji
mkubwa wa kushinda Uchaguzi Mkuu.
Kauli ya Nape inaungwa mkono na Mwenyekiti wa
Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Simba aliyesema CCM haiteteleki
kutokana na muungano wa Ukawa kwa kuwa ina mtaji wa wapigakura wengi.
“CCM tunajivunia kwa sababu Watanzania bado wana
matumaini nasi, lakini hata kwa umoja wetu kama chama, tumefika vijijini
tofauti na chama chochote, hao wapinzani wanakomea mjini tu,” alisema
Simba.
Hata hivyo, mwenyekiti mstaafu wa UWT, Anna
Abdallah alitoa maoni yake kwa tahadhari akisema kigezo pekee na muhimu
kuliko vyote kitakachoifanya CCM kurejea madarakani ni uteuzi wa mgombea
anayekubalika kwa wananchi, kwa kuwa huo ndiyo mtaji mkubwa kuliko
vyote.
Alisema CCM imewahi kufanya makosa katika uteuzi wa majimbo kadhaa na kuchukuliwa upinzani.
“Kuchagua anayekubalika ni kigezo kikubwa kuliko
vyote, kuhusu habari nyingine ya tuhuma au vigezo sita, sioni kama zina
mashiko sana. Waswahili wanasema, “ukimpenda Mmakonde basi penda na
ndonya yake”, alisema akimaanisha ukikipenda chama, penda na
makandokando yake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni