Timu ya Azam imesema ina imani ya
kutetea ubingwa wa Tanzania Bara ikiwa tayari kuwakaribisha wagonga
nyundo kutoka jijini Mbeya, Mbeya City katika uwanja wa Chamazi, nje
kidogo ya jiji la Dar es Salaam Jumatano wiki hii.
Msemaji wa Azam, Jafari Idd amesema lengo ni kushinda na hatimaye kuongoza tena ligi hiyo.Azam, iliyoanzishwa mwaka 2007, ipo nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 36 wakati wapinzani wao, Mbeya City wapo nafasi ya 7 wakiwa na pointi 24.
Mbeya City, ikicheza ligi kuu kwa msimu wa pili, ilifanya vizuri sana msimu wake wa kwanza uliopita ikimaliza nafasi ya tatu huku Azam wakiwa mabingwa, lakini msimu huu, ilianza kwa kusuasua na baade kukaa vizuri.
Hata hivyo, Azam inabidi isali sala zote kuiombea Yanga isishinde mechi yake ya leo dhidi ya Coastal Union itakayochezwa katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam ili kuipunguza kasi.
Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 40 na imedhamiria kuifunga Coastal Union (iliyo nafasi ya 6-pointi 24) ili kuendelea kuweka pengo la uongozi kati yake na Azam na wapinzani wao wa jadi, Simba wakiwa nafasi ya tatu na pointi 35.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni