Watu 20 wameuawa mashariki mwa Nigeria kufuatia mashambulizi mapya yanayoendeshwa na kundi la Boko Haram katika eneo hilo.
Eneo
la kwaJaffa, katika jimbo la Borno, lilishambuliwa Jumapili jioni na
washambulizi hao waliowashambulia wananchi na baadaye kuteketeza nyumba
zao.Majuma machache yaliyopita miji kadhaa na vijiji vilikombolewa na wanajeshi wa Nigeria wakisaidiwa na Chad, Cameroun na Niger.
Mwanamume aliyetoroka mji wa Kwajaffa wakati wa mashambulizi ya kundi hilo la Boko Harram amerudi nyumbani kwake na kupata kumeharibika pakubwa.
Aliambia BBC kuwa alihesabu maiti za raia waliokuwa wamepigwa risasi na wanamgambo wa Boko Harram na alipata maiti zingine zilizokuwa zimeteketezwa.
Shambulio hilo linadhaniwa kuwa adhabu kwa jamii nzima kwa sababu karibu nyumba zote ziliteketezwa.
Boko Haram lina tabia ya kulenga maeneo ambayo raia wameunda makundi ya ya kiusalama ambayo wakati mwingine hushirikiana na wanajeshi wa Serikali.
Vijiji viwili katika eneo la Kala Balge lililo karibu na mpaka na Cameroon pia vilishambuliwa na watu 14 waliuawa.
Washambulizi hao wamefukuzwa katika miji na vijiji vingi na jeshi la muungano wa mataifa jirani ambayo yangali nchini humo.
Hata hivyo mauaji ya hivi karibuni yanaonyesha kuwa raia wengi wangali katika hatari ya kushambuliwa wakati wowote.
Zaidi ya watu milioni moja waliotoroka makwao bado hawawezi kurudi nyumbani kwa sababu hakuna usalama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni