Watawala nchini Thailand wamekamata kilo 250 za pembe za ndovu zilizokuwa zimefichwa ndani ya kasha moja iliyotokea Afrika.
Meno hayo 130 na bidhaa zingine zilizochongwa kutoka kwa pembe ya tembo zilikuwa zikisafirishwa kuelekea Laos kutoka Jamhuri ya Congo kupitia Addis Ababa Ethiopia.
Naibu mkurugenzi wa halmashauri ya ushuru nchini Thailand Chamroen Photiyod,alisema kuwa pembe hizo ziligunduliwa zilipopandishwa ndege ya kuingia nchini humo huko Ethiopia na hivyo wakaweka mtego ulionasa furushi zima la pembe.
''Shehena hiyo ilikuwa imeorodheshwa kama bidhaa ya thamani ya juu na ilikuwa imefungwa ndani ya makasha mawili ya mbao''alisema bwana Photiyod
Maafisa wa forodha katika uwanja wa ndege wa Suvarnabhumi ulioko Bangkok ndio waliokamata shehena hiyo haramu yenye thamani ya dola laki tatu.
Hii ni mara ya 11 kwa maafisa nchini Thailand kukamata pembe za ndovu zenye thamani kubwa zikijaribu kuingizwa katika soko la Asia ambapo bidhaa zinazotokana na pembe za ndovu
zinathamaniwa sana.
Wawindaji haramu wameua maelfu ya ndovu katika bara la Afrika katika jitihada ya kufaidika kutokana na utashi wa bidhaa zinazotokana na pembe za ndovu hususan katika soko la Asia.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni