Mamlaka nchini Kenya imesema kuwa walinda usalama wamekabiliana na washukiwa wa kundi la wapiganaji wa kiislamu la Al- Shaabab, katika wilaya ya Ijara katika kaunti ya Garissa Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.
Mapema, wapiganaji hao waliokisiwa kuwa zaidi ya 50 kutoka Somalia, wanasemekana kushambulia kambi za polisi katika eneo la Yumbis, takriban kilomita 30 kutoka Daadab.
Wavamizi wa Al-Shabaab waliteka vijiji vitatu na kupeperusha bendera yao Kaskazini Mashariki mwa Kenya kwa muda kabla ya maafisa wa polisi nchini kenya kuwasili na kuwafurusha.
Vijiji vilivyovamiwa ni Ramu iliyoko Mandera, na vijiji vya Yumbis na Holugho vilivyoko Garissa.
Walioshuhudia wamesema kuwa wapiganaji hao waliikejeli serikali ya Kenya na wakawaonya wanavijiji kwa kuendelea kushirikiana na serikali ya Kenya.
Japo viongozi nchini Kenya wamesema kuwa maafisa wa usalama wamewafurusha wanavijiji wenyeji wa Yombis wanadai kuwa bado wapiganaji hao wako.
Tukio hilo linawadia siku moja tu baada ya wapiganaji wa kundi hilo kuvamia msikiti mjini Garissa.
Wapiganaji hao waliwahutubia waumini waliokuwa msikitini kwa karibu saa mbili kabla ya kutokomea mwituni.
Waliikosoa serikali ya Kenya na kuonya waumini dhidi ya kuwa majasusi wa serikali ya Kenya.
Mwezi uliopita Al Shaabab walivamia chuo kikuu cha Garissa na kuwaua watu 150 wengi wao wanafunzi.
Kundi hilo kutoka Somalia linaaminika kuwa na wafuasi nchini Kenya ambapo limetekeleza mashambulizi kadha katika jitihada ya kuilazimisha serikali ya Kenya kuondoa majeshi yake nchini Somalia.
Majeshi ya Kenya ni miongoni mwa kikosi cha kulinda amani cha muungano wa Afrika Amisom ambao wanaisaidia serikali dhaifu ya Somalia kupigana na waasi wa Al Shabaab.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni