Uongozi wa serikali mpya ya rais Muhamadu Buhari ambayo itaingia madarakani siku ya ijumaa wiki hii inaulaumu utawala unaondoka wa Goodluck Jonathan kwa kuhujumu taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika.
Uongozi wa All Progressives Congress (APC) unailaumu utawala uliopoa sasa kwa ukosefu mkubwa wa mafuta ukosefu wa umeme na upungufu wa uzalishaji kutokana na migomo inayoendelea ya wafanyikazi na deni kubwa la taifa.
APC inailaumu PDP kwa kuiwacha taifa hilo katika hali mbaya ya kiuchumi na hivyo kuhujumu utawala unaotarajiwa kushika hatamu karibuni.
Kwa mujibu wa msemaji wa APC Lai Mohammed,''hii ndiyo mara ya kwanza katika historia ya taifa hilo kwa serikali kupeana mamlaka huku uchumi ukiwa katika hali mabaya zaid''
''Kwa sasa uchumi wetu ambao ndio mkubwa zaidi barani Afrika unadeni kubwa la dola milioni 60 nao wafanyikazi wamegoma wakidai mabilioni ya fedha.
''Umeme haupo na mafuta pia ambayo ndio nguzo ya uchumi haipo kwa kweli uchumi umekwama''aliongezea Lai.
Kwa upande wache chama cha rais anayeondoka Goodluck Jonathan PDP kimekanusha madai ya kuhujumu uchumi wa Nigeria.
Msemaji wa rais Goodluck Reuben Abati,aliwashukuru wanigeria kwa kumpa fursa ya kuwaongoza .
Kupitia kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter alituma ujumbe kwa niaba ya rais Goodluck ambaye alihudhuria misa yake ya mwisho akiwa rais na akawaaga wafuasi wao.
Msemaji wa chama chake Olisa Metuh naye aliwaonya wanachama wa chama cha Buhari kukoma kuichafulia jina chama cha PDP.
Bwana Metuh alisema si kweli kuwa PDP kimehujumu uongozi na uchumi wa Nigeria
'' Imekuwaje kuwa katika utawala wa rais Goodluck hakujatokea ukosefu kama huu wa mafuta na umeme ''?
''Nahisi kama kuna watu wenye ushawishi katika serikali inayokuja ambao wanataka kuzua hali ya taharuki na kuibua madai kuwa hawakurithi kitu chochote katika akiba ya serikali''.
Mwandishi wa BBC aliyeko Nigeria anasema kuwa chanzo cha uhaba huo mkubwa wa mafuta na umeme ni mashirika na makampuni yanayoagiza mafuta ambayo yameamua kususia kuingiza mafuta yakidai malimbikizo ya pesa wanazodai serikali.
Jenerali mstaafu Buhari alishinda uchaguzi wa urais wa Nigeria katika uchaguzi uliofanyika tarehe 28 mwezi Machi na kuipa chama cha upinzani ushindi wake wa kwanza katika historia ya taifa hilo.
Buhari ameratibiwa kuchukua uongozi wa taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta ijumaa ijayo.
Majuzi kampuni zinazotoa huduma za simu zilitangaza kuwa zimelazimika kutumia mafuta kuzalisha umeme hatua ambayo ni ghali na kuwa hazingemudu gharama zake.
Nigeria ambayo huzalisha takriban mapipa milioni mbili ya mafuta kila siku haina vinu vya kusafishia mafuta nchini humo na inalazimika kuagiza mafuta kutoka nje.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni