Maafisa wa serikali Mashariki mwa China wamelazimika kuzuru gereza moja nchini humo kama ilani ya kutoshiriki ufisadi.
Maafisa hao 70 wakiwa wameambatana na wachumba wao walilazimishwa kushinda mchana kutwa katika gereza moja lililoko mjini Shiyan katika mkoa wa Hubei tarehe 15 mwezi Mei.
Serikali kuu ya China ilianzisha harakati za kukabiliana na ufisadi miongoni mwa wafanyikazi wa uma tangu rais aliyeko madarakani Xi Jinping alipochukua mamlaka mwaka wa 2012.
Tangu mwaka huo 2012, maelfu ya wafanyikazi wa uma wamechunguzwa na asilimia kubwa yao kuhukumiwa jela baada ya kupatikana na hatia ya kutumia madaraka yao vibaya.
Ziara hiyo ya lazima iligundulika baada ya shirika la kupambana na ufisadi kuchapisha ripoti hiyo katika jarida lake la hivi punde siku ya jumamosi.
Kulingana na ripoti hiyo ya tume ''ziara hiyo ilipaswa kuwaonya na kuwapa fursa ya kuonja maisha ndani ya jela nyuma ya vyuma vikubwa na madirisha yaliyoweka juu zaidi''
Picha zilizochapishwa zinaonesha maafisa hao wakuu wa umma wakiambatana na wachumba wao.
Maafisa hao walipata fursa ya kuzungumza na maafisa wanaotumikia vifungu tofauti kwa makosa ya ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka yao.
Aidha walitembelea maonyesho ya picha na maandishi ya wafanyikazi wenza waliofungwa.
Tume hiyo ya kupambana na ufisadi CCDI ilisema katika ripoti hiyo kuwa wengi wa maafisa hao walipigwa na butwaa walipowaona maafisa waliowahi kufanya kazi pamoja na wengine wakawachwa vinywa wazi baada ya kuwatambua vigogo waliotamba katika enzi zao lakini sasa wakiwa ni wafungwa.
Maafisa hao walilazimishwa kusikiza sauti za maafisa waliowatangulia wakikiri makosa yao.
China imekuwa ikiendesha kampeini kubwa ya kupambana na ufisadi na ubadhirifu wa mal ya uma huku maafisa wa uma wakitakiwa kuishi maisha yao kadri ya mishahara yao.
Aisha wafanyikazi wa umma wametakiwa kukoma kupokea zawadi ghali kutoka kwa wanakandarasi na watu wenye nia ya kufanya biadhara na serikali.
Vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti visa ambayo maelfu ya wafanyikazi wadogo serikalini wanakamatwa na kilele cha kampeini hiyo dhidi ya ufisadi ilikuwa kukamatwa kwa aliyekuwa mkuu wa usalama wa ndani Zhou Yongkang.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni