Mbeya. Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku
amesema si dhambi kwa wananchi kupiga kura ya hapana Katiba
Inayopendekezwa.
Akizungumza juzi jioni kwenye mdahalo wa Katiba
ulioandaliwa na taasisi hiyo ambao ulifanyika katika ukumbi wa Chuo
Kikuu cha Teofilo Kisanji (Teku) jijini Mbeya, Butiku alisema kura ya
Hapana au Ndiyo, zote zinatoa fursa sawa kwa wananchi kuamua kwa utashi
wao.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na mamia ya
wakazi wa Mbeya, Butiku aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, alieleza kuwashangaa viongozi wa
vyama na Serikali kuwachagulia wananchi kura ya Ndiyo.
Akitolea mfano wa chama chake cha CCM, Butiku
alisema hakitakiwi kuwahadaa Watanzania na kuwataka kuipigia kura ya
Ndiyo katiba hiyo, badala yake kiwaache waamue wenyewe.
Aliwataka wananchi watumie muda huu kuitafuta
nakala ya Katiba Inayopendekezwa, waisome na kuielewa ili hatimaye
waamue ama kuipigia kura ya Hapana au Ndiyo.
“Mchakato huu una mambo makuu mawili ya kuamua
ambayo ni kura ya Ndiyo au Hapana. Hivyo basi kupiga kura ya Hapana siyo
dhambi kwani inatoa nafasi kwetu sote kukaa tena na kuangalia upungufu
uliojitokeza na kilichosababisha upungufu huo nini ili tusirudie tena
makosa,” alisema Butiku na kuongeza:
“Kura ya ndiyo inamaanisha tunaikubali Katiba
Inayopendekezwa, hata ikiwa haina mashiko itaendelea kutumika kwa vile
mmeikubali, lakini nisisitize kwamba kura ya hapana siyo dhambi, ipo
kisheria na asije mtu akawaambia mpigie kura ya ndiyo.
Alisema kabla ya kuipitisha au kuikataa Katiba
Inayopendekezwa ni vyema ikashindaniwa kwa hoja na si kwa nguvu au ngumi
huku akiwataka vijana nchini kutothubutu kujiingiza kwenye mikumbo
inayoweza kusababisha nchi ikaingia kwenye machafuko.
Profesa Baregu
Akizungumza katika mkutano huo, Profesa Mwesiga
Baregu ambaye pia alikuwa mjumbe wa tume hiyo, alisema licha ya Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuahirisha Kura ya Maoni ya Katiba
Inayopendelezwa kwa muda usiojulikana, kwa mtazamo wake anaona
haitakuwapo kabisa.
“Mimi Baregu, nasema hivi siyo kwamba
imeahirishwa, nafikiri haitakuwapo kabisa kura hiyo na hii inatokana na
ambavyo mchakato mzima ulivyoendeshwa na si kwa maudhui yaliyomo kwenye
Katiba Inayopendekezwa, bali ni kwa namna ambavyo Bunge Maalumu la
Katiba lilivyofanya na uandishi wake.”
Alisema katu Watanzania wasije wakawa na papara na
Katiba hiyo hata baada ya Uchaguzi Mkuu, bali wawe na subira kwani
wakiiendea haraka inaweza ikaipeleka nchi mahala pabaya na kujikuta
ikitumbukia kwenye machafuko yasiyo na tija.
Hamphrey Polepole
Mjumbe mwingine wa tume hiyo, Hamphrey Polepole
alisema Watanzania wanatakiwa kutambua kwamba Katiba siyo kitu cha
kuamuliwa na wanasiasa au kuamua kwa kusikia tu, bali ni kwa kushiriki
katika kuipigia kura ya hapana au ndiyo kwa kutumia utashi wao binafsi.
“Katiba hii siyo ya wanasiasa ni ya wananchi
wenyewe, lakini cha kushangaza hapa ni wanasiasa wanavyochukua nafasi
kubwa ya kuuteka mchakato huu na hii yote wanataka wapate nafasi ya
kulinda masilahi yao na kuendelea kututawala watakavyo, hivyo ndugu
zangu wa Mbeya na Watanzania wote chukueni hatua.”
Alisema anawashangaa hata viongozi wakubwa ndani
ya vyama na Serikali kuendelea kuipigia ‘debe’ Katiba Inayopendekezwa
kwa kuwahadaa wananchi kupiga kura ya ndiyo wakati wakitambua fika
kwamba haijakidhi matakwa Watanzania.
Mjumbe mwingine wa iliyokuwa Tume hiyo, Ally Saleh
alizungumzia masuala ya muundo wa Serikali, alishangiliwa na mamia ya
watu waliofurika ukumbini hapo aliposema: “Mwenyekiti wangu hapa
(Butiku) kasema kwamba kura ya hapana siyo dhambi, lakini mimi nasema
hivi, watu wasipige kabisa kura.”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni