Dar es Salaam. Hofu ya kuahirishwa kwa Uchaguzi
Mkuu imezidi kutanda baada ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) na wanaharakati kueleza kuwa kuna dalili ndogo za
uchaguzi huo kufanyika Oktoba.
Lakini mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji Damian
Lubuva amesema viongozi wa kisiasa wasiwajaze wananchi hofu isiyo na
sababu kwa kuwa ofisi yake imeongezewa uwezo wa kuandikisha wapigakura
na hivyo wana uhakika kazi hiyo itakamilika kabla ya Oktoba.
“Vifaa vimeanza kuwasili. Tumeshapata mashine za
(Biometric Voters Registration) BVR 248, nyingine 1,600 zinatarajiwa
kuwasili wakati wowote kuanzia sasa na Serikali imeshalipia mashine
zote,” alisema Jaji Lubuva.
“Kwa hiyo kadri muda unavyokwenda, ndivyo uwezo
wetu wa kusajili unavyokuwa mkubwa zaidi na inawezekana tukamaliza kabla
ya Julai.”
Kuhusu kusimamia kauli yake kuwa Kura ya Maoni
ingefanyika kama ilivyopangwa lakini ikahirishwa baadaye, Jaji Lubuva
alisema wasingeweza kuahirisha mapema kabla ya kuona ugumu wa kazi
yenyewe.
Lakini viongozi wa vyama vya upinzani wanaona
ahadi hizo ni kama ilivyokuwa kabla ya kuahirishwa kwa Kura ya Maoni na
kwamba kasi ndogo ya uandikishaji wapigakura inaweza kusababisha
Uchaguzi Mkuu kuahirishwa.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba,
mwenyekiti Chadema Freeman Mbowe, mwenyekiti wa NLD Emmanuel Makaidi na
mkurugenzi wa asasi ya kiraia ya Concern For Development Initiative in
Africa (Fordia), Bubelwa Kaiza, wana hofu ya Uchaguzi Mkuu kuweza
kufanyika Oktoba.
Alichosema Lipumba
Akifungua mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF,
Profesa Lipumba alisema vifaa vilivyowasili ni vichache kulinganisha na
mahitaji ya Tume.
Kuna giza nene
“Hadi sasa daftari la wapigakura halijakamilika
hata katika mkoa mmoja na bado vifaa vingi havijawasili nchini,” alisema
Lipumba ambaye alidokeza kuwa suala hilo litakuwa ajenda kwenye kikao
hicho cha siku mbili.
Profesa Lipumba alisema walipokwenda Kenya kwa
ajili ya ziara ya mafunzo, walielezwa na Tume ya Uchaguzi ya Kenya
kwamba kazi ya uandikishaji wapigakura inatakiwa kuchukua angalau mwaka
mmoja.
Profesa Lipumba alisema kwa namna ambavyo Jaji Lubuva hayuko
huru, Ukawa ina wasiwasi kama mgombea wao wa urais anaweza kutangazwa
mshindi iwapo atashinda.
Lipumba alisema NEC waliiomba Serikali BVR 15,000
ili kuandikisha wapigakura kwa urahisi, lakini Serikali ikapunguza na
kuidhinisha vifaa 8,000.
Jumla ya wapigakura milioni 24 wanatarajiwa kujitokeza kujiandikisha kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Mbowe ndiye aliyekuwa wa kwanza kueleza hofu hiyo.
Akizungumza na Mwananchi mwishoni mwa wiki,
mwenyekiti wa Chadema, Mbowe alisema inaonekana Serikali ya Awamu ya Nne
haijajiandaa kuachia madaraka na hivyo kuna uwezekano wa kuomba
iongezewe muda.
“Hadi sasa hakuna tunachojua wala kuelezwa. Hofu
yetu ni kwamba Serikali inaweza kuomba iongezewe muda kwa kuwa usajili
wa wapigakura hautakamilika,” alisema.
“Kama uandikishaji wapigakura wa mwaka 2010
ulifanyika mwaka mmoja kabla, hawa watawezaje kukamilisha katika miezi
mitano tu tena kwa kuandikisha kwa BVR?”
Makaidi
Naye Makaidi alisema jana kuwa NEC inachelewesha
uandikishaji wa wapigakura kama mbinu ya kuruhusu Serikali iliyopo
kuongezewa muda wa kukaa madarakani.
Makaidi, ambaye anadai ameshapitishwa na NLD
kugombea urais, alisema haiwezekani vifaa vichelewe kuja nchini wakati
kazi ya uandikishaji wapigakura ilishajulikana muda mrefu.
“NLD tunasema mbinu hizo tumeshazigundua, NEC
ifanye haraka kuandikisha wapigakura ili uchaguzi ufanyike Oktoba na si
vinginevyo, ucheleweshaji huu wa makusudi utawagharimu,” alisema.
Fordia haioni dalili za uchaguzi
Mkurugenzi wa Fordia, Buberwa Kaiza pia alisema haoni dalili za
Uchaguzi Mkuu kufanyika mwaka huu kutokana na maandalizi yake kuchelewa.
Kaiza alisema ukata unaoikabili NEC na kuchelewa
kwa maandalizi ya msingi ya utoaji wa elimu ya uraia, vinatoa picha kuwa
mambo yanaenda mrama kuelekea Uchaguzi Mkuu.
“Nina shaka kuwa uchaguzi unaweza kuahirishwa kama
ilivyotokea kwa shughuli ya Kura ya Maoni, kwa sababu naona maandalizi
yamechelewa sana. Kwa kawaida, maandalizi ya Uchaguzi Mkuu hufanyika
mwaka mmoja na nusu kabla,” alisema Kaiza.
“Imebaki miezi mitano maandalizi hayajafanyika
kikamilifu, sasa kama unataka kufanya uchaguzi huru na haki utawezaje
kufanya maandalizi ya mwaka mmoja na nusu ndani ya miezi iliyobaki na
wakati huo ukikabiliwa na uhaba wa fedha?”
Kitendo cha NEC kuchelewa kulipia mashine za BVR
na kuziingiza nchini mashine hizo kwa awamu, kitafanya uandikishaji
kuchelewa zaidi kwa kuwa mashine zilizopo ni moja ya nane tu ya mashine
zote zinazotakiwa.
“Kwa vyovyote vile uandikishaji utakwenda hadi
Oktoba kwa sababu ni mkoa mmoja tu wameshafanya hadi sasa, bado
hawajafundisha wataalamu wa kuendesha mashine, hawajasafiri kwenda
maeneo ya uandikishaji. Kuna matatizo ya kiufundi.
“Kwa namna gani wanaweza kufika mwezi Oktoba
wakiwa wamemaliza kusajili, kuhakiki na kuthibitisha majina na NEC ikawa
tayari kusimamia uchaguzi na mambo mengine?”
Mrema ataka uchaguzi uahirishwe
Hata hivyo, mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alikuwa na mtazamo tofauti ingawa anakiri kuwa maandalizi yanasuasua.
Mrema aliiambia Mwananchi jana kuwa katika mkutano
uliofanyika Dodoma mwaka jana baina ya Rais Jakaya Kikwete na viongozi
wa upinzani chini ya mwamvuli wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD),
alishauri Uchaguzi Mkuu uahirishwe, lakini alitazamwa vibaya na viongozi
wenzake wa upinzani.
“Wengine walihoji ‘huyu kibaraka anasema nini?’
Najua kuna ambao waliona huyu kikaragosi anataka kutuharibia mambo
yetu,” alisema.
“Ambaye alinitazama vizuri ni Rais Kikwete pekee
yake wengine wote walinitazama vibaya kabisa na nafikiri hata rais
aliniona huyu naye sijui karogwa, lakini hakusema kitu,” alisema.
Mbunge huyo wa Vunjo, alisema sasa kuna kila dalili kuwa uchaguzi mkuu kufanyika Oktoba ni jambo gumu.
“Nilisema siku hiyo na kupuuzwa, lakini hicho
ndicho ambacho kinajitokeza sasa,” alisema na kuongeza kuwa mchakato wa
uandikishaji katika Daftari la Wapigakura kwa teknolojia ya BVR
umekwama.
Pia mchakato wa kuunda Katiba, nao huenda
usikamilike kwa wakati na kwamba hata kama Kura ya Maoni itapigwa,
itakuwa ngumu kwa taratibu zote kukamilika, ikiwa ni pamoja na
marekebisho ya sheria na kanuni.
“Katiba ikipita kuna sheria na kanuni ambazo
zitahitaji mabadiliko, wabunge ni lazima wakakutane kwa ajili hiyo hivyo
sidhani kama muda utatosha hivyo ni wazi kuwa ili mambo yaweze kwenda
sawa, ni lazima uchaguzi uahirishwe,” alisema.
Alisema, Rais Kikwete amechoka na kuwa katika
nafasi hiyo urais ni jambo gumu, kuna changamoto nyingi na sasa
angependa kupumzika.
Hata hivyo, alisema kabla ya kuahirisha Uchaguzi
Mkuu, Serikali ni lazima ifanye majadiliano na wadau badala ya
kukurupuka, kitu ambacho alisema kinaweza kusababisha mgogoro.
“Wakiahirisha bila kushirikisha wadau, hasa (mwenyekiti wa DP,
Christopher) Mtikila, wasubiri kesi Mahakama Kuu,” alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni