Morogoro. Watu 18 wameteketea kwa moto baada ya basi la Kampuni
ya Nganga Express na lori aina ya Fuso kugongana uso kwa uso na kuwaka
moto katika eneo la Iyovi, Milima ya Uduzungwa, Morogoro
Katika ajali hiyo iliyotokea jana saa mbili
asubuhi, abiria 15 waliokuwa kwenye basi na wengine watatu wa lori
waliteketea kwa moto huku wengine 10 wakijeruhiwa vibaya.
Taarifa na picha za ajali hiyo zilianza kusambaa
jana asubuhi kupitia mitandao ya kijamii zikionyesha masalia ya miili ya
walioteketea.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul
alisema ajali hiyo ilitokea baada basi hilo lililokuwa linatoka
Kilombero kwenda Mbeya likiwa kwenye mistari ya barabarani ya katazo na
kwenye mwendo kasi kugongana na lori lililokuwa limebeba matikiti na
kuwaka moto.
Alisema majeruhi wanne wamelazwa katika Hospitali ya St. Kizito, Mikumi na sita wako katika Hospitali ya Mtandika, Iringa.
Alisema kwenye basi hilo kulikuwa na pikipiki ambayo pia iliungua na kusema inawezekana ndiyo iliyosababisha moto huo.
Ajali hiyo ni mfululizo wa ajali zinazotokea
katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni siku moja baada ya watu watano
kufariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mikoa ya Dodoma na
Iringa saa 36, baada ya kumalizika mgomo wa madereva nchini.
AJALI MWAKA HUU
Aprili 9: Basi la Ngorika lililokuwa likitokea Dar
es Salaam kwenda Arusha liligongana na basi la Ratco lililokuwa
likitokea Tanga kwenda Dar es Salaam baada ya gari ndogo aina ya Toyota
Passo iliyokuwa ikitokea Korogwe kuelekea Dar es Salaam kupoteza
mwelekeo na kusababisha vifo vya watu 10.
Aprili 3: Ajali ya basi dogo la mashabiki wa klabu
ya Simba SC Tawi la Mpira na Maendeleo (Simba Ukawa) eneo la
Makunganya, Morogoro ilisababisha vifo vya watu saba na kujeruhi 24.
Machi 11: Watu 50 walifariki dunia na 22
kujeruhiwa katika ajali baada ya lori kugongana na basi la abiria la
Kampuni ya Majinjah Express eneo la Mafinga Changarawe, mkoani Iringa.
Machi 22: Watu wawili walikufa na 22 kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Itamboleo, wilayani Rujewa, Mbeya.
Februari 26: Watu watatu walifariki dunia papohapo baada ya lori
la mafuta walilokuwa wamepanda kupinduka na kuwaka moto eneo la Wedi,
katika Kijiji cha Maseyu mkoani Morogoro.
Januari 15: Watu wanne walifariki dunia baada ya
basi la Hajees kupinduka katika Kijiji cha Mnazi, Kata ya Mandela
wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni