Staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platinumz’ amefungukia
msimamo wake juu ya mwandani wake wa zamani, Wema Sepetu ‘Madam’ kwa
kusema kuwa kamwe hawezi kumrudia tena.
Licha ya Diamond kufunguka hayo, wawili hao wamekuwa na mapenzi ya
vipindi, kuna wakati waliwahi kumwagana kisha kurudiana na hakuna
aliyewahi kutoa tamko zito lakini safari hii Diamond amesema ndiyo basi
tena!
Kwa mujibu wa chanzo makini cha gazeti la Risasi kilicho karibu na
staa huyo, mara kwa mara Diamond amekuwa akijiwekea nadhiri ndani ya
moyo wake na kusisitiza kwamba pamoja na kuwa maisha ya sasa huendeshwa
kwa msingi wa fedha lakini hata kama ‘atafulia’ kiasi gani, ni bora afe
maskini kuliko kurudiana na Wema.
“Diamond amekuwa akisema kila wakati kwa msisitizo kuwa kutokana na
matatizo aliyokumbana nayo katika uhusiano wake kwa Wema, ni vigumu sana
kurudiana naye wala kuwaza kama ipo siku anaweza kuwa naye, maana
hakuna tena jambo geni asilolijua kwake,” kilisema chanzo hicho na
kufunguka zaidi:
“Kama hiyo haitoshi, Diamond anasema anaposema haoni kitu kipya kwa
Wema anamaanisha ndiyo maana utaona leo hakuna hata siku moja ambayo
amewahi kuwaza kurudiana naye hata kama atatumia ushawishi wa fedha kwa
kumpelekea makontena ya fedha, hawezi kukubali anasema bora afe maskini
kuliko kushea kitanda kimoja na Wema.”
Baada ya madai hayo, gazeti hilo lilifanya jitihada za kukutana na
Diamond uso kwa uso ambaye alithibitisha taarifa ambazo zilielezwa na
mtu wake wa karibu:
“Umeambiwa na nani hayo? Sipendi kuongelea sana hivi vitu lakini huo
uliousikia ndiyo ukweli. Kwa sasa nawaza maisha yangu na mpenzi wangu
Zari baada ya kupitia majaribu mengi kimapenzi enzi hizo.
“Huenda wengi wasiamini ninayosema lakini nafsi yangu haijawahi
kuniongoza kukumbuka ya nyuma tena kama ilivyowahi kutokea awali.
“Wengi wamekuwa wakiniuliza swali kama hili lakini sikupenda kujibu
kwa kuwa nilihisi litaleta tafrani kwa mashabiki wangu, sioni sababu ya
kuendelea kuulizwa kwenye media hivyo ukweli ni kwamba siwezi kurudi
nyuma tena,” alisema Diamond.
Kuonesha kweli amedhamiria kutogeuka nyuma, Diamond alisema kwa sasa
yuko bize studio kurekodi wimbo na Nay wa Mitego (Emmanuel Elibariki)
ambao utakuwa umesheheni majibu ya maswali yote ya kila kitu ambacho
kilimkera kwenye uhusiano wake na Wema.“Naomba mashabiki wangu wawe na
subira kwa maswali hayo yote, majibu yake yatapatikana katika project
yangu na Nay inayokuja muda si mrefu,” alisema Diamond.
Alipotafutwa Wema kuhusiana na kauli hiyo ya Diamond, naye alijibu
mashambulizi kwa kusema kamwe hawezi kurudiana na Diamond, hamfai hata
kidogo na hata akimshawishi na fedha nyingi kiasi gani hawezi kurudi
nyuma.
“Hata aje na Bill Gates (tajiri mkubwa duniani), aje na matajiri wote
anaowajua yeye duniani kamwe siwezi kulamba matapishi, kwanza sitaki
kukumbuka kabisa kuhusu huyo mtu, please naomba nisimuongelee kabisa
huyo mtu,” alibwatuka Wema.
Picha: Wema na Diamond enzi za penzi lao
11 Aprili 2015
Diamond Atoa Kiapo, Wema Ajibu Mapigo
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni