Wahamiaji haramu wasiopungua 400 wanahofiwa kuzama katika bahari ya Meditarrania, baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kupinduka nje ya pwani ya Libya.
Shirika la kimataifa la uhamiaji IMO na lile la hisani la Save the Children yamesema kati ya manusura 144 na 150 waliwasili katika mji wa Reggio Calabria uliyoko kwenye ncha ya kusini kabisaa mwa Italia Jumanne asubuhi.
Save the Children ilisema katika taarifa ikiwanukuu manusura hao, kwamba kulikuwepo na wahanga 400 wa ajali ya boti hiyo, na kufafanua kuwa miongoni mwa waliookolewa ni pamoja na wavulana na watoto wadogo.
Msemaji wa IMO nchini Italia Flavio Di Giacomo aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP, kwamba manusura kadhaa waliliambia shirika lake kuwa kulikuwepo na watu kati ya 500 na 550 kwenye boti hiyo wakati ilipozama. Uchunguzi wa awali unaashiria kuwa boti hiyo huenda ilizama baada ya abiria kuanza kutembea baada ya kuiona timu ya uokozi ya Italia.
Wakimbizi waliookolewa wakiwasili katika bandari ya Porto Empedocle katika jimbola Sicily siku ya Jumatatu.
Mjadala waibuka upya Italia
Janga hilo la karibuni linakuja wakati maafisa nchini Italia wakisema karibu wahamiaji 8,500 waliokolewa baharini kati ya Ijumaa na Jumatatu, na hivyo kuwasha upya mjadala nchini Italia, juu ya iwapo nchi hiyo ina wajibu wa kuwapokea na kuwahifadhi wahamiaji wote wapya wanaowasili.
Kuboreka kwa hali ya hewa katika bahari ya Mediterrania hivi karibuni kumesababisha ongezeko la wahamiaji wanaojaribu kuwasili nchini Italia kwa kutumi boti. Hali inayozidi kuwa ya machafuko nchini Libya, eneo muhimu wanakoanzia safari wakimbizi, pia imechochea ongezeko la watafuta hifadhi wanaojaribu kufika barani Ulaya.
Serikali ya Italia inasema zaidi ya wahamiaji 15,000 wamewasili mpaka sasa katika mwaka huu wa 2015. Wizara ya mambo ya ndani ya Italia imeziamuru wilaya zote za kanda kutafuta makaazi ya dharura kwa ajili ya wahamiaji 6 500 -- hatua iliyokosolewa na upinzani, ambao unahoji kuwa sera ya kuwaokoa wahamiaji inawapa moyo wengine kujaribu safari hiyo hatari.
Wapinzani Italia watishia kugoma, Ugiriki yajiandaa
Kiongozi wa chama kinachopinga wahamiaji cha Northern League Matteo Salvini, aliwataka viongozi wa serikali za wilaya kutoka chama chake kukataa kuwapokea wahamiaji wapya, akiandika kwenye ukurasa wake wa facebook kuwa chama hicho kiko tayari kuzikalia hoteli, mabweni, shule na hata kambi zilizoandaliwa kwa ajili ya wimbi jipya la wakimbizi.
Ugiriki ilisema siku ya Jumanne kuwa inapanga kuunda vituo vya mapokezi bara, kushughulikia wimbi jipya la wahamiaji kutoka visiwani. Uamuzi huo katika kikao cha dharura cha baraza la mawaziri kilichoongozwa na waziri mkuu Alexis Tsipras, ulifikiwa baada ya wahamiaji na wakimbizi zaidi ya 700 hasa kutoka Syria na Waafrika kuwaili nchini Ugiriki kati ya Ijumaa na Jumanne.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,dpae
Mhariri: Grace Patricia Kabogo
Mhariri: Grace Patricia Kabogo
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni