Ni mfano wa kirusi kilichokosa jina ambacho kinasambaa na
kuathiri wanafunzi wengi wanaofikiria na kuamini kuwa ‘kupiga chabo’
(kuibia katika mtihani), ni njia pekee inayoweza kuwakomboa katika
masomo yao.
Siku chache zilizopita, taarifa zilisambaa
mitandaoni kuhusu tukio la wazazi 300 waliokamatwa na kufunguliwa
mashtaka nchini India, baada ya kukutwa katika vituo vya kufanyia
mitihani, wakitumia njia mbalimbali kuvujisha majibu kwa watoto wao
waliokuwa wakifanya mitihani yao ya mwisho.
Wazazi hao walikamatwa baada ya kunaswa na mtego
wa kamera ulioonyesha mkanda wa video wa tukio hilo lililotokea katika
jimbo la Bihar.
Kutokana na tukio hilo, wanafunzi zaidi ya 700
wamefutiwa matokeo wa mtihani huo ulioandaliwa na Bodi ya Mitihani ya
jimbo la Bihar(BSEB).
Hali ilivyokuwa
Waziri wa Elimu nchini India, PK Shai, alisema
hali hiyo isingeweza kuondolewa kwa nguvu ya serikali pekee kutokana na
ukubwa wa tukio, kwani watu watatu mpaka wanne walionekana wakitoa
majibu ya mtihani kwa mwanafunzi mmoja.
Kwa mujibu wa picha zilizosambazwa kwenye
mitandao, ikiwamo iliyotumika katika makala haya, wazazi wanaonekana
wakiwa katika madirisha ghorofani wakitafuta njia za kuwapa watoto wao
majibu.
Funzo kwa Tanzania
Vitendo vya udanganyifu kwenye mitihani, ni tatizo
la kidunia. Kwa Tanzania, wachambuzi wanasema wapo wazazi
wanaoshirikiana na walimu na hata wamiliki wa shule kuiba mitihani kwa
minajili ya kuzipa shule jina kwa kufaulisha.
Mwalimu mkuu wa Shule ya Sekondari Chiungutwa,
iliyopo Wilaya ya Masasi vijijini, Hamza Nampoto, anataja sababu tatu
zinazosababisha uvujishaji wa mitihani kwa wanafunzi.
Sababu ya kwanza anataja kuwa ni mikataba ya
ukuzaji wa viwango vya ufaulu inayotolewa kati ya shule na uongozi wa
elimu kama vile wilaya au mkoa. Mikataba hii anasema inawashawishi
walimu kufanya udanganyifu kwa sababu za kuwaridhisha wakubwa au
kuepukana na adhabu.
“Mwalimu mkuu inabidi atumie namna yoyote ile ili
kuhakikisha shule yake inafaulisha ili angalau aweze kufikia kile
kiwango alichoagizwa na Mkurugenzi au Katibu tawala wa Mkoa,’’ anasema.
Sababu ya pili anasema ni baadhi ya wazazi wanaotaka watoto wao wapande madaraja ya elimu pasina kujali kama wana uwezo au la.
‘’Pia hata mazingira ya rushwa kwa wasimamizi
yamekuwa yakitawala, kuna wasimamizi ambao wanaamini kupata nafasi hiyo
ni kumaliza shida zao kwa kuuza mitihani,’’anataja sababu ya tatu.
Mzazi Maria Mwemezi, anasema chanzo kikuu cha
udanganyifu kwenye mitihani, ni mfumo wa ajira unaopigia zaidi chapuo
ubora wa vyeti badala ya maarifa na ujuzi wa wahitimu.
Anasema hakuna ofisi yeyote iliyo tayari kuajiri mfanyakazi asiyekuwa na vyeti vizuri, kama anavyofafanua:
“Kabla ya kuangalia uwezo au uzoefu wa mfanyakazi,
mwajiri huangalia zaidi cheti, kwa hivyo inashawishi hata wazazi
kutumia mbinu zote kuhakikisha watoto wao wanafaulu.’
Kaimu Mkurugenzi wa shirika la HakiElimu, Godfrey
Boniventura, anasema wanafunzi wengi vyuoni hawasomi kwa bidii, bali
wanasubiri kuvuja kwa mitihani
‘’Maana ya kwenda shule siyo kutafuta vyeti bora,
bali ni kuhakikisha mwanafunzi anapata maarifa ya kutosha, uwezo wa
kujiamini katika kazi anayoifanya na mawasiliano ya kujieleza mbele ya
watu, ‘’anasema.
Athari ya ufaulu unaotokana na kufanya
udanganyifu, anasema ni kuwapo kwa Watanzania katika soko la ajira ambao
vyeti vyao havifanani uwezo walionao.
“Unakuta mwanafunzi ana cheti kizuri cha chuo
kikuu lakini hawezi hata kujieleza, sasa unajiuliza alipata vipi cheti
hicho. Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, bado tunaburuzwa na wenzetu
katika soko la ajira ukiacha Burundi inayoshika nafasi ya mwisho, sasa
tunaelekea wapi?”anahoji.
Elimu kugeuzwa biashara
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania
(CWT), Ezekiah Oluoch anasema jambo jingine linalosababisha wizi kwenye
mitihani ni ushindani wa shule kufaulisha kwa minajili ya kuvutia soko
la wateja (wanafunzi).
“Shule zimekuwa biashara na biashara ni matangazo,
ili upate wateja ni lazima ufaulishe sana. Kwa hivyo, inakubidi kutumia
mbinu zote kufaulisha kwa kiwango cha juu,” anasema na kuongeza:
“Hata hivyo, kwa miaka mitano sasa sijasikia uvujishaji wa
mitihani, kwa sababu Necta wamefunga mianya kwa asilimia zote kwa shule
za umma na binafsi.
Anasema shule nyingi zinajitangaza kwa viwango vya
ufaulu, hususani katika matokeo ya kidato cha nne na sita. Kutokana na
mazingira hayo, wazazi wengi wamekuwa wakishawishika kupeleka watoto
katika shule hizo.
Mtazamo wa kitaalamu
Mwaka 2000, aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la
Mitihani Tanzania (Necta), Dk Joyce Ndalichako, alisema mitalaa ya
elimu nchini inachangia kwa kiasi kikubwa kuwapo kwa udanganyifu katika
mitihani.
Alilitazama suala hili kuanzia namna ya uandaaji
wa walimu, uelewa wa mitalaa, mazingira ya kufundishia na kujifunzia,
menejimenti za shule na pia matarajio ya jamii katika elimu.
Akizungumza katika mkutano wa 20 wa Chama cha
Tathmini ya Elimu Barani Afrika (AEAA) uliofanyika mkoani Arusha, Dk
Ndalichako wakati huo akiwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
alisema kila kipengele kinawachochea wanafunzi, wazazi na walimu
kujiingiza katika udanganyifu.
Ufumbuzi wa tatizo
Katika mada yake aliyoitoa kwa wajumbe: Jinsi
uwasilishaji mitalaa unavyochochea udanganyifu wa mitihani Tanzania, Dk
Ndalichako alipendekeza ili kuhakikisha mfumo wa mitihani unakuwa wa
haki, kuna haja ya kuwa na mpangilio mzuri wa mitalaa, mbinu za
ufundishaji na mitihani yenyewe.
Pia alishauri kuwapo kwa walimu wazuri, wanafunzi wanaofundishwa vizuri na mazingira mazuri ya kujifunzia.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni