WAZIRI
Mkuu Mizengo Pinda, ameshiriki kikamilifu kubomoa misingi ya taifa
hili. Ni kutokana na kutaka kuwapo Mahakama ya Kadhi nchini. Anaandika Eberi M. Manya … (endelea).
Ameahidi ndani ya Bunge Maalum la Katiba, kuundwa kwa mahakama hii na
sasa anajitahidi kadri awezavyo kuhakikisha inapatikana sasa.
Siyo kesho wala kesho kutwa. Muswada juu ya mahakama hiyo, uko njiani kuingia bungeni.
Pinda anasema, Mahakama ya Kadhi itakayoundwa, itashughulikia mirathi na ndoa. Basi!
Wapo wanaofananisha harakati za Pinda za kutaka kuingiza Mahakama ya
Kadhi nchini na mbio zake za kusaka urais kama alivyoeleza katika
tangazo lake la kimyakimya.
Ikiwa
ni hivyo, basi atakuwa anafanya makosa makubwa sana. Urais haupatikani
kwa kughiribu Waislamu. Urais unapatikana kwa mtu kuwa mkweli, mwadilifu
na mwenye uwezo wa kusimamia kile unachokinena. Pinda hana sifa hizo.
Pinda
tayari amelikoroga. Kauli yake kuwa Zanzibar sio nchi, ni kikwazo
kingine katika mbio zake hizi. Kuruhusu kuwapo Mahakama ya Kadhi ndani
ya mgawanyiko kati ya waumini wa Kiislamu na Kikirsto, ni kutenda makosa
kama ambayo, Rais Yoweri Museveni aliyafanya nchini kwake mwaka 1986.
Alirejesha utawala wa kifalme katika eneo la Baganda. Utawala
wa Kabaka ulikuwa umefutwa na watangulizi wake. Museveni alidhani kumpa
Kabaka hadhi yake ya ufalme, kungesaidia kuishi kwa amani zaidi.
Miaka
minne baadaye, maafisa wa mamlaka ya kodi walipoenda Buganda kukusanya
kodi katika eneo hilo ambalo linahusisha jiji la Kampala, wakaambiwa
Rais Museveni hana mamlaka juu ya eneo hilo. Kodi wakasema wanalipa kwa
Kabaka.
Tatizo
hilo bado lingalipo hadi leo. Serikali inalazimika kupigana vita ya
ndani kwa ndani kwa sababu tu mfalme Kabaka hatambui mamlaka ya
serikali.
Tunafahamu
“sakata” la mahakama ya Kadhi lilipoanzia. Limeletwa na serikali ili
kuwalainisha Waislamu, kupigia kura ya “Ndiyo” Katiba pendekezwa.
Yawezekana dhamira ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi ilikuwa njema, lakini mkondo iliyopitia kutaka kuiunda, haukubariki.
Mahakama hii inaletwa kama rushwa kwa Waislamu.
Hatua
ya hukumu za mahakama hiyo kusajiliwa katika mahakama kuu au waziri
mwenye dhamana na masuala ya sheria kuthibitisha maamuzi ya mahakama
hiyo, ni kuingiza dini katika utendaji wa serikali.
Dini
zote zinapaswa kujiendesha kwa sadaka au michango ya waumini wao. Kama
Mahakama ya Kadhi itaanzishwa, kuna siku serikali italazimika
kuidhinisha, kulipia na kugharamia mahakama za makanisa.
Aidha,
kuruhusu ujio wa Mahakama ya Kadhi, tena kufanya kazi zake kwa kutumia
kodi za wananchi wote, kutachagiza, kufunguliwa milango kwa Wakristo
kutaka kesi zao ziishie madhabahuni.
Ndani
ya Kanisa Katoliki kwa mfano, kuna sheria – Canon Laws – ambazo ni
kali mno. Wakristo wanaokengeuka huadhibiwa kwa kunyimwa huduma zote za
kanisa (excommunication).
Tukifikia
hapo nchi hii haitatawalika tena. Maelezo kwamba kesi za Waislamu
zikihukumiwa na mahakimu au majaji wakristo hawazifahamu vyema sheria za
Kiislamu hayana mashiko. Sheria za Kiislamu au (Islamic Law) kwa yeyote
aliyesoma sheria anaisoma.
Mfumo
wetu wa kutoa haki ambao Ibara ya 107 A ya Katiba ya Jamhuri tumeitumia
kwa miaka zaidi ya 50 sasa, hakujawa na kasoro, zinazohalalisha kuundwa
kwa mahakama hii.
Tukiingiza
imani katika uendeshaji wa nchi kwa matarajio kuwa ama tutapigiwa kura
na Wakristo au Waislamu; ama mtu kutaka urais, tutaitumbukiza nchi
katika vurugu.
Ni bora Pinda akose urais ikiwa nia yake ni hiyo; lakini taifa libaki salama.
Tayari maaskofu wameshatoa tamko lao la kupinga mahakama ya kadhi. Nimesikia baadhi ya viongozi wanawabeza.
Mwandishi
wa makala hii, amejitambulisha kuwa ni msomaji wa mtandao huu na
mtafiti wa masuala ya kisiasa. Anapatikana kwa simu namba 0785 510536,
barua pepe: ebermanya@yahoo.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni