Dar es Salaam. Serikali imetishia kuanza
kutekeleza sheria inayodhibiti asasi za kijamii na kidini, ikizitaka
taasisi hizo kuacha mara moja kutoa matamko yanayolenga kuwashawishi
waumini wao waikatae Katiba Inayopendekezwa na pia kuwapangia nini cha
kufanya katika Uchaguzi Mkuu ujao na kusema watakaobainika watachukuliwa
hatua kali.
Katika kuzipiga ‘kufuri’ taasisi hizo, Serikali
imesema kuanzia Aprili 20 itazifuta taasisi zote zilizosajiliwa na
Wizara ya Mambo ya Ndani ambazo havifuati matakwa ya kisheria ya
kuwasilisha taarifa zao za mwaka za ukaguzi wa hesabu na kulipa ada za
kisheria.
Hata hivyo, viongozi wa dini ya Kikristo na
Kiislamu waliozungumza na gazeti hili jana kuhusu kauli hiyo, wamesema
taasisi zao zinawakilisha watu, na hivyo zina haki ya kikatiba na
kisheria kupinga jambo lolote zitakaloona linakwenda kinyume na maslahi
ya Taifa na kwamba ziko tayari kukaguliwa.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe alisema
jana kuwa kazi hiyo ya kupitia usajili wa vyama hivyo itaanza kwa vyama
vilivyopo jijini Dar es Salaam, baadaye kuendelea nchi nzima. Vyama
vyote vitakavyofutiwa usajili vitawekwa katika tovuti ya wizara hiyo na
havitaruhusiwa kuendelea na shughuli zake.
“Matukio ya aina hii yanapofanyika yanaashiria
kuvuruga amani na utulivu nchini. Kazi ya Serikali ni kuhakikisha
usalama wa watu wote unaimarishwa ili shughuli zote za kisiasa, kidini,
kijamii na kiuchumi, zinatekelezwa kwa misingi ya kisheria,” alisema
Chikawe.
Uamuzi huo umekuja wakati Jukwaa la Wakristo
likiwa limetoa tamko la kuwataka waumini wake kujiandikisha kwa wingi
katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, kuisoma Katiba Inayopendekezwa
na kujitokeza kuikataa kwa kupiga kura ya hapana.
Jukwaa hilo, linaloundwa na Jumuiya ya Kikristo
Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) na
Umoja wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (CPCT), linadai kuwa Serikali
imewaahidi Waislamu kuwapa Mahakama ya Kadhi ili waipigie Katiba
Inayopendekezwa kura ya ndiyo. Jambo ambalo limesema litasababisha
mgawanyiko.
Mbali na jukwaa hilo, pia Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu liliwataka waumini wake kuikataa Katiba Inayopendekezwa iwapo
Serikali itashindwa kuwasilisha bungeni muswada wa Mahakama ya Kadhi ili
chombo hicho kitambulike kisheria. Muswada huo uliondolewa baada ya
kuibuka kwa mvutano mkali katika mkutano wa 19 wa Bunge uliomalizika
Aprili Mosi, mwaka huu.
Katika siku za hivi karibuni viongozi mbalimbali
wa dini wamekuwa wakitaja wazi sifa na hata majina ya watu wanaopaswa
kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu ujao, na wakati fulani vikundi vya
wachungaji na masheikh kwa nyakati tofauti vilienda nyumbani kwa kada wa
CCM, Edward Lowassa mjini Dodoma kumshawishi atangaze nia ya kugombea
urais.
“Kauli za viongozi wa dini kuhusu masuala ya
Katiba au Uchaguzi Mkuu ujao zinakiuka sheria za usajili wa taasisi zao.
Viongozi ambao tayari wameshatoa matamko ya aina hiyo tunawapa onyo kwa
sasa, wasirudie tena,” alisema Waziri Chikawe.
Alisema waumini wana haki ya kuamini mafundisho ya
dini zao, lakini wanapaswa kutekeleza masuala yao ya kisiasa na kijamii
kwa utashi wao bila ya kushawishiwa na mtu yeyote, kama sheria za nchi
zinavyotaka.
“Mfano ni pale kiongozi au viongozi wa dini
wanapochangisha fedha za kuandamana au kukutana na wanasiasa kwa kile
kinachoelezwa kuwa ni kuwashawishi kugombea nafasi mbalimbali za
uongozi. Hii si kazi ya taasisi za dini na ni kinyume na sheria,”
alisema.
Alisema wananchi, vikundi na taasisi za dini zinatakiwa kuepuka
kushiriki katika vitendo ambavyo vinaashiria kuvuruga amani na utulivu
nchini.
“Serikali itachukua hatua kali kwa watu binafsi,
vyama vya siasa na taasisi za dini zitakazobainika kuvuruga usalama na
utulivu wa nchi, ikiwa ni pamoja na kuvifuta katika daftari la usajili
wa vyama vya kijamii ambavyo vitakiuka Katiba ya kuanzishwa kwake,”
alisema.
Viongozi wa dini wajibu
Wakizungumzia kauli hiyo ya Serikali, viongozi wa dini walikosoa tamko hilo wakisema linalenga kuwafumba midomo.
“Ninachoamini, taasisi zote zipo kwa mujibu wa
sheria. Kama Serikali inataka kuzibana hizi taasisi zisifanye kazi kwa
uhuru wake, itunge sheria nyingine ya kuzibana, hata hizo sheria mpya
tutahakikisha zinapitiwa na kujadiliwa kabla ya kupitishwa. Tupo tayari
kufanyiwa ukaguzi,” alisema katibu wa CCT, Dk Leonard Mtaita. Alisema
jumuiya hiyo inawakilisha watu ambao ndio inawasemea, hivyo haina hofu
yoyote juu ya kuendelea kufanya kazi zake kwa uhuru na kungalia maslahi
ya taifa.
Naibu katibu wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislam na
Shura ya Maimam, Rajab Katimba alisema: “Kutengeneza tishio kwa taasisi
ni kutaka kuzifumba mdomo kwa sababu Televisheni ya Taifa (TBC)
inahamasisha kura ya ndiyo kuhusu Katiba, wakiwemo wabunge na viongozi
wa serikali.”
Alisema hakuna dhambi yoyote iwapo taasisi mbalimbali zitawaeleza Watanzania ukweli wa yaliyomo katika Katiba Inayopendekezwa.
“Kukagua ni haki yao. Viongozi wa dini wanayo haki
ya kutokubaliana na jambo lolote ambalo wataona halina maslahi kwa
Taifa. Tutapinga tu haitakuwa haki kukubaliana na kitu ambacho hakina
maslahi kwa Watanzania, eti tu kwa hofu ya kufungiwa,” alisema.
Naye Sheikh Khamis Mataka, ambaye ni katibu mkuu
wa Taasisi ya Masheikh Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, Sheikh alisema:
“Taasisi za dini zinalea na kuwajenga kiroho waumini. Lengo la serikali
wakati wote lionekane kuziimarisha na si kutengeneza mazingira ya
kuzifunga mdomo.”
Wanasheria
Akizungumzia kauli hiyo, mwenyekiti wa Baraza la
Katiba Zanzibar, Profesa Abdul Sheriff alisema hizo ni dalili za
Serikali kuongeza petrol kwenye moto.
“Dalili zilianza kuonekana muda mrefu jinsi
serikali ilivyoanza kuongeza petroli katika moto, inataka kufanya jambo
la hatari kwa kuzifumba mdomo taasisi mbalimbali,” alisema Profesa
Sherrif.
Alisema kufutiwa kwa usajili kwa vyama hivyo ni taratibu za
kisheria na si agizo la kisiasa, na kwamba hakuna taasisi yoyote ambayo
itakuwa tayari kuogopa tishio la Serikali kwa kuwa itapinga mahakamani.
Mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC), Hellen-Kijo Bisimba aliona tamko hilo kuwa ni woga wa
Serikali.
“Ninachokiona ni hofu na woga tu kwa sababu
Serikali inajua nguvu ya taasisi katika ushawishi wake kwa wananchi.
Zinaweza kukwamisha mipango ya serikali,” alisema.
Alisema Serikali inataka kuzifungia taasisi hizo wakati ikijua wazi kuwa kila raia ni sehemu ya siasa.
“Sijui wanaitafsiri vipi siasa? Ninachofahamu ni
kuwa kila raia yupo ndani ya siasa? (Serikali) Inajaribu kutaka kutumia
nguvu kupitisha maslahi yake,” alisema.
Waziri Chikawe alisema jijini Dar es Salaam jana
kuwa onyo hilo pia linawagusa watu binafsi na vyama vya siasa
vinavyobeba wanachama wake kutoka eneo moja kwenda jingine kuhudhuria
mikutano ya hadhara, akisema kuwa jambo hilo ni chanzo cha vurugu na
linatakiwa kuachwa mara moja.
Chikawe pia alipiga marufuku tabia ya vyama vya
siasa ya kubeba wanachama kutoka eneo moja kwenda jingine kuhudhuria
mikutano ya hadhara kwa maelezo kuwa hali hiyo imekuwa chanzo cha
vurugu.
“Utekelezaji wa jambo hili utapunguza ushabiki wa
kisiasa na pia tatizo la uvamizi wa wanachama wanapokuwa wanatoka kwenye
mikutano ya mbali na maeneo hayo. Kwanza tutapunguza mzigo wa ulinzi
kwa askari wetu. Huwezi kutoa watu Mbagala kuja katika mkutano Gongo la
Mboto,” alisema.
Chikawe pia aligusia suala la ugaidi akisema
Serikali imejipanga kukabiliana nalo, ikiwa ni pamoja na kuwafuatilia
watu wote wanaoingia na kutoka nchini, huku akiwataka wazazi kuwa karibu
na watoto wao ili wasijiingize katika vitendo hivyo.
“Jeshi letu ni imara sana katika nchi za Afrika Mashariki na ya Kati. Msiwe na wasiwasi tupo salama sana,” alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni